Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewakamata waganga wa kienyeji 55 wakiwa na viungo vya binadamu vikiwamo meno na nywele vinavyodaiwa kuwa ni vya watu wenye albino. Vitu vingine walivyokutwa navyo ni ngozi ya simba, nyumbu, mamba, vibuyu, njuga, vioo, shanga na debe tatu za bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema waganga hao walikamatwa katika wilaya za Mkoa wa Mwanza kwenye msako ulioanza juzi. Alisema katika msako huo wamefanikiwa kuwakamata waganga hao wanaodaiwa kupiga ramli chonganishi zinazosababisha kuchochea matukio ya mauaji kwa albino na vikongwe.
“Katika msako wa Jeshi la Polisi ulioanza juzi tumefanikiwa kuwatia mbaroni waganga wa jadi 55 ambapo kati yao tumewakuta na nywele, meno za watu wenye albino waliouawa katika matukio tofauti mkoani hapa,” Mlowala.
Kamanda huyo wa Polisi alisema waganga hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ikiwamo kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria pamoja na viungo vya binadamu.
Mbali na tukio hilo, taarifa kutoka wilayani Misungwi zinaeleza kuwa watu wanne wamefikishwa kortini mjini hapa kwa tuhuma za kuuza mafuta maalumu ya ngozi yanayotumiwa na watu wenye albino. Mafuta hayo yenye thamani ya Sh milioni tano, ambayo yalitolewa na Hospitali ya Bugando kwa watoto wenye albino wilayani humo.
0 comments:
Post a Comment